Header Ads

WAISLAM WAKUMBUSHWA KUHESHIMU IMANI ZA WENGINE

Waumini wa dini ya kiislam mkoani humu (Lindi) wamekumbushwa wajibu wao wa kuheshimu imani za watu wengine ili kudumisha mshikamano.

Wito huo ulitolewa jana mjini Lindi, na katibu wa baraza la amani la viongozi wa dini wa mkoa wa Lindi, Abdilahi Salum wakati maadhimisho ya kumbukumbu ya kuuwawa kwa mjukuu wa mtume Muhmmad S.A.W, imam Hussain.

Shehe Abdilahi alisema ili kudumisha mshikamano na amani iliyopo nchini, jamii inatakiwa kuheshimu imani ya kila mmoja ambapo waislam wanatakiwa kuwa mfano bora wa kuheshimu imani za wengi.

 Alisema jamii ikijenga utamaduni wa kuheshimu imani ya kila mmoja kutakuwa na mshikamano utakaosababisha kuwepo amani ya kudumu na upendo baina yake.

''Kuheshimu imani ya mwenzako ni alama ya ustaharabu. Kwahiyo ni rahisi watu wa imani nyingine kukuamini na hata kujiunga na imani yako,'' alisema shehe Abdilahi.

Katibu huyo alisema jamii inatakiwa kutambua kwamba amani ni chanzo kikubwa cha maendeleo, kwani mahali pasipo na amani hapawezi kuwa na utulivu unaoweza kusababisha kufanyika shughuli za maendeleo na uchumi.

 Kwa upande wake msemaji wa dhehebu la Shia Khoja Ithnaasheri Jaamat katika kumbukizi hiyo, ustadhi Mohamed Manguli alitoa wito kwa waislam kuandika wosia ili kuepusha migogoro inayotokana na kugombea mali, pindi wanapofariki dunia.

 Alisema  migogoro ni chanzo cha kuvuruga amani na utulivu  katika jamii ambayo inaweza kufanya shughuli za maendeleo na uchumi kwa ufanisi iwapo itaepukwa.

No comments

Karibu tena,asante kwa kusoma habari hii!