Header Ads

TEMBO WAVAMIA MAKAZI YA WATU NA KUHARIBU MALI NA VYAKULA

Kundi la Tembo zaidi ya 10 wamevamia makazi ya watu na kuharibu nyumba, mali na vyakula vya aina mbalimbali katika kijiji cha Halawa kata ya Nkidwabiye wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.

Jumla ya kaya 11 zimekosa chakula wala mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kuvamiwa na tembo hao.

Licha ya nyumba hizo kuharibiwa, tembo hao pia  wameharibu chakula chote kilichohifadhiwa ndani ya nyumba hizo.

Tembo hao  waliotoka katika pori la akiba Maswa, wanadaiwa kuvamia kijiji hicho usiku wa kuamkia jana Septemba Mosi,  saa saba usiku, ambapo waliezua nyumba 11 za familia saba zenye watu zaidi ya 50.

Mtendaji wa kijiji hicho Mayenga Matongo amesema tembo hao walivamia kaya hizo  na kuezua nyumba zote 11 na kula mahindi magunia 42, viazi magunia sita huku akibainisha kuwa hakuna vifo vilivyotokea.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga alisema inashangaza kuona Tembo wamebadilika kwa kuanza kula vyakula vinavyoliwa na binadamu, huku akiwataka viongozi wa pori la akiba la Maswa kubadili mfumo wa ulinzi kwa Tembo hao kutokana na wanyama kubadilika.

Kiswaga pia amewataka wananchi kujenga nyumba bora na za kudumu ambazo haziwezi kubomolewa na wanyama hao huku akiwaahidi serikali itahakikisha inaendelea kulinda wananchi na mali zao.

"Serikali inafanya tathimini ya athari iliyofanywa na Tembo ili kulipa fidia kwa wathirika walioko nje ya mita 500 kutoka kwenye mpaka, ila walioko ndani ya mita 500 hawatalipwa fidia kwa sababu wamevamia pori," amesema Kiswaga.


Mkuu huyo wa wilaya akiwa ameambatana na Viongozi wa CCM wilaya, walifika eneo la tukio na kutoa pole kwa wananchi hao pamoja na kukabidhi msaada wa chakula ambao ni unga wa mahindi kilo 220, maharage kilo 50 na sukari kilo 20.

No comments

Karibu tena,asante kwa kusoma habari hii!