Header Ads

IMANI POTOFU CHANZO CHA BAADHI YA WAKAZI MKOANI SHINYANGA KUJISAIDIA VICHAKANI.


MKUU WA MKOA WA SHINYANGA BI.ZAINAB TELLACK

SHINYANGA
Na Salvatory Ntandu (Kijukuu Blog)
Kaya elfu 7,195  katika  mkoa Shinyanga zimebainika kutokuwa na vyoo  na kuendelea kujisaidia vichanani hali ambayo inaweza kusababisha kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kama vile homa za matumbo na hata kipindupindu.

Hayo yamebainishwa leo na Afisa Mazingira wa mkoa wa Shinyanga Neema Simba, katika ufunguzi wa kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha ujenzi wa vyoo bora ijulikanayo kama “usichukulie poa nyumba ni choo” ambayo imeanza rasmi katika mkoa huo.

Amesema kuwa mwaka 2012 hali ya vyoo bora ilikuwa asilimia 17 na baada ya utekelezaji kampeni ya ujenzi wa vyoo bora imeboreka na kufikia  asilimia 50.6 ambapo malengo ya mkoa ni hadi kufikia desema mwaka huu kila kaya iwe na choo bora.

Amefafanua kuwa Halmashauri ya Mji wa kahama ina asilimia 75 vyoo bora ni asilimia 0.2 hazina vyoo, Halmashauri ya Kishapu asilimia 71 vyoo bora asilimia 2 hazina vyoo,Halmashauri ya Msalala asilimia 57.3 vyoo bora asilimia 4.4 hazina vyoo.

Halmashauri ya Shinyanga vijijini asilimia 19.7 vyoo bora asilimia3.9 hazina vyoo.Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga asilimia 64 vyoo bora asilimia 0.9 hazina vyoo,Halmashauri ya Ushetu asilimia 20.9 vyoo bora asilimia 5.1

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack amewaagiza wakurugenzi wote wa Mamlaka za serikali za mitaa katika mkoa huo kutoa elimu kwa wananchi wanaoendelea na mila potofu ikiwemo ya kutochangia choo kimoja na wakwe hali ambayo inasababisha wananchi kuendelea kujisaidia vichakani na kuchafua mazingira.

Nae Elizabeth Malingumu Afisa mwelimishaji kutoka wizara ya afya na maendeleo ya jamii wazee jinsia na watoto amesema malengo ya kampeni hiyo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 kila nyumba hapa nchini iwe na afya bora na kuwataka wananchi wa mkoa wa shinyanga kuhakikisha wanajenga vyoo bora.

Kampeni ya nyumba ni choo itadumu kwa siku 22 katika mkoa wa shinyanga ambayo inaongozwa na balozi mkuu Msanii Mrisho Mpoto ambapo watazunguka katika halmashauri sita za mkoa huo ambayo inalenga kuhamasisha ujenzi wa vyoo bora.

MATUKIO KATIKA PICHA:

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mhe. Zainab Telack akitoa onyo kwa wanasiasa kuingilia oparesheni ya ukaguzi wa choo kwa kila nyumba na kuwakingia kifua wale ambao watakutwa hawana vyoo kwa madai ni wapiga kura wao.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko, akizungumza akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Nyumba ni choo ambapo amesema wataisimamia na kuhakikisha inafanikiwa kwa wananchi wote kuwa na vyoo bora.

Awali Afisa Afya wa mkoa wa Shinyanga Neema Simba akisoma taarifa ya usafi wa mazingira ya mkoa wa Shinyanga. ametaja Takwimu kuwa kati ya kaya za mkoa wa Shinyanga 284,701 wanaotumia vyoo ni asilimia 50.6 na wasio na vyoo ni asilimia 5.5.

Mratibu wa uhamasishaji wa kampeni hiyo kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Elizabeth Malingumu akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Nyumba ni choo. Amesema wamezindua kampeni hiyo ili kuhamasisha wananchi wote wa mkoa wa Shinyanga wanakuwa na vyoo bora kwenye nyumba zao.

Mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la uholanzi (SNV) Elisekile Bwile, akielezea namna wanavyosaidiana na Serikali kuhakikisha nchi ya Tanzania wananchi wake wanakuwa kwenye mazingira ya usafi pamoja na kufadhili kujenga miradi ya kuhifadhia maji taka ukiwamo na mji wa Shinyanga.

Balozi wa kampeni ya nyumba ni choo msanii Mrisho Mpoto akizungumza na wananchi wa mkoa wa Shinyanga na kuwataka wajenge vyoo bora, vilivyoezekwa mapaa juu, milango pamoja na kuwepo na maji ya kunawa mikono.

Diwani wa Kata ya Kambarage manispaa ya Shinyanga Hassan Mwendapole akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo ya nyumba ni choo.

Awali Katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Albert Msovela, akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo ya nyumba ni choo, kabla ya kuanza kutambulisha viongozi mbalimbali wa Serikali.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack katikati, akiwa na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko (wa kwanza kushoto), pamoja na katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Albert Msovela kabla ya kuzindua kampeni hiyo ya nyumba ni choo.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack awali kabla ya kwenda kwenye viwanja vya Zimamoto kuzindua kampeni ya nyumba ni choo akipiga picha ya pamoja na Balozi wa uhamasishaji wa kampeni hiyo Mrisho Mpoto kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa.


No comments

Karibu tena,asante kwa kusoma habari hii!