Header Ads

DC KAHAMA ATOA ONYO KWA WAFANYABIASHARA WAKUBWA KUTOWATUMIA WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO KUPITIA VITAMBULISHO VYA JPM.

MKUU WA WILAYA YA KAHAMA ANAMRINGI MACHA.

KAHAMA

SERIKALI wilayani Kahama mkoani Shinyanga imetoa onyo kwa wafanyabiashara wakubwa Wilayani humo wenye mpango wa kuwatumia wafanyabiashara ndogondogo kuwauzia bidhaa zao mitaani kwa kutumia vitambulisho vya Ujasiliamali vilivyotolewa na Rais John Pombe Magufuli.

Onyo hilo limetolewa leo Mjini Kahama na mkuu wa Wilaya ya Kahama Anamringi Macha wakati akizindua vitambulisho vya ujasiliamali kwa halmashauri za Kahama Mjini,Msalala na Ushetu.

Macha amesema wamepata taarifa kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wameanza kuwaambia wafanyabiashara ndogondogo wakiwemo wamachinga watafute vitambulisho hivyo ili wawape bidhaa wauze mitaani kwa kuwa ukiwa na kitambulisho hicho hulipi kodi wala usumbuliwi na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA).

Ameongeza kuwa nia ya wafanyabiashara hao ni ovu na kwamba kufanya hivyo ni kuiibia Serikali kwa kukwepa kulipa kodi halali na kusema kuwa mfanyabiashara mdogo  akikutwa na bidhaa hizo za dukani ataombwa risiti na wakaguzi  kisha kufikishwa katika vyombo vya Sheria yeye na mtu aliyempatia bidhaa hizo.

Katika hatua nyingine Macha amesema wataunda madawati maalumu kwa halmashauri ya Msalala,Kahama Mji na Ushetu ili Kurahisisha  wajasailimali wadogo kuchukua fomu za kuomba vitambulisho hivyo katika maeneo waliyopo.
 KUSHOTO NI MKURUGENZI WA HALMASHAURI YA MJI WA KAHAMA ANDERSON MSUMBA AKIWA NA MKURUGENZI WA HALMASHAURI YA MSALALA SAIMON BEREGE.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya Msalala Saimon Berege amesema kuwa vitambulisho hivyo vitasaidia kuwatambua kihalali wajasilimali wadogo katika halmashauri na kuleta wepesi wa kuwapatia mikopo na kuwakwepa wafanyabiashara wadanganyifu wanaoomba mikopo licha ya kuwa mitaji yao ni mikubwa katika biashara zao.

Naye mkurugenzi wa Halmashauri ya Kahama Mji,Anderson Msumba amewataka wajasilimamali wadogo  kutoa taarifa sahihi katika fomu walizopewa na kuongeza kuwa kupitia vitambulisho hivyo itasaidia kuweka mikakati mizuri ya kuwainua wajasiliamali hao kutoka daraja la Chini kwenda la kati hadi kufikia daraja la juu.

Awali wakitoa maoni yao baadhi ya wafanyabiashara wadogo wilayani Kahama wamempongeza Rais Magufuli kwa kuja na mpango huo na kuongeza kuwa vitambulisho hivyo vitawasaidia kufanya biashara zao kwa amani tofauti  na ilivyokuwa zamani  ambapo walikuwa wanasumbuliwa na kudharauliwa. 

Wilaya ya Kahama imepatiwa vitambulisho elfu kumi katika awamu ya kwanza,ambavyo vitatolewa katika halmashauri ya Kahama Mjini,Halmashauri ya Msalala na Halmashauri ya Ushetu.

No comments

Karibu tena,asante kwa kusoma habari hii!