Header Ads

MCHUNGAJI MSIGWA ASEMA KUHAMIA DODOMA SI KIPAUMBELE CHA TAIFA

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema) Mchungaji Peter Msigwa amesema uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma haukuwa sahihi kwasababu si kipaumbele cha Taifa.

Amesema pia jambo hilo halimo katika mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano.

Akizungumza bungeni leo Jumanne Septemba 4, 2018 katika mjadala wa muswada wa sheria ya kulitangaza Jiji la Dodoma kwa Makao Makuu ya nchi mwaka 2018, Mchungaji Msigwa amesema kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ni dhana nzuri lakini kuna tofauti kubwa ya kufanya jambo zuri na sahihi.

“Inaweza kuwa jambo zuri lakini lisiwe sahihi sisi kama wabunge ni wajibu wetu kusimamia kodi za serikali,” amesema.

“Kwa hiyo masuala mengi tunayoletewa na Serikali ni wajibu wetu kutafakari kwa pamoja kama Taifa kwamba hili suala tunalokwenda kulifanya is it economical.”

Amesema kuwa wengi wa wabunge wanasema Mwalimu Julius Nyerere alishawahi kusema kuhusu Dodoma kuwa makao makuu lakini ukweli ni kwamba amesema mambo mengi.

“Ameshawahi kusema kuwa chama kinachofuata kutawala baada ya CCM ni Chadema mbona na hili nalo hamlitekelezi? Hatuwezi kusema mambo yote aliyosema mwalimu Nyerere tuyatekeleze,”amesema.

Amesema Tanzania ina matatizo mengi na kuhoji kwa kupima mizani suala la kuhamia Dodoma ni kipaumbele cha Taifa na kwamba suala hilo halikuwa katika mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano wala wa mwaka mmoja.

No comments

Karibu tena,asante kwa kusoma habari hii!