Header Ads

MANGULA AZINDUA KAMPENI ZA UBUNGE MONDULI.....JINA LA LOWASSA LATAWALA

Makamu mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula jana amezindua kampeni za ubunge wa Monduli jijini Arusha huku, jina la Lowassa likitawala.

Wakizungumza katika mkutano wa kampeni hizo, zilizofanyika uwanja wa soko la Monduli, viongozi wengi wa CCM isipokuwa, Mangula walilazimika kulitaja jina la Lowassa wakati wakieleza sababu za aliyekuwa mbunge wa Chadema wa jimbo hilo kujiunga na CCM.

Viongozi hao walirejea kauli zao kuwa, Lowassa yupo njiani kurudi CCM na waliohama wamemtangulia tu.

Edward Lowassa ni waziri mkuu wa zamani ambaye alihamia Chadema mwaka 2015 na jana alikuwa Mto wa Mbu jimboni humo akizindua kampeni za Ubunge kwa kumnadi Yonas Laiser.

Aliyekuwa mwenyekiti wa halmashauri ya Monduli na Diwani wa Monduli mjini, Isack Joseph ambaye hivi karibuni alijiuzulu udiwani na kujiunga CCM, alisema kabla ya uamuzi huo alikwenda mara tatu kuonana na Lowassa.

Joseph alisema katika safari zake kwa Lowassa alimweleza ni vigumu kwao kama madiwani wa Monduli kuendeleza maendeleo aliyoacha kwani wapo upinzani. Alisema alichomwambia muda bado wa wao kuondoka Chadema wasubiri hadi mwaka 2019.

"Mimi ndiye nilikuwa rafiki wa karibu wa Lowassa hapa Monduli, nilimwambia, sisi kuendelea kuwa Chadema ni kuwaumiza wananchi kwani hakuna msaada wowote kutoka Chadema," alisema.

Alisema Chadema inapokea ruzuku zaidi ya Sh390 milioni kila mwezi lakini imeshindwa hata kuajiri makatibu wa wilaya ama kujenga hata zahanati.

"Tumeamua kurejea CCM kujali maslahi ya wana Monduli na wala hatujamsaliti Lowassa kwani na yeye yupo njiani anakuja" alisema.

Kwa upande wake, mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kama ambavyo amekuwa akieleza, Lowassa yupo njiani kurudi na watampokea.

Alisema Lowassa anawachezea wananchi wa Monduli kwani anajua yeye bado ni waziri mkuu mstaafu ambaye anatembelea gari la Serikali, analindwa na walinzi wanaolipwa na Serikali.

Alisema yeye kama mkuu wa mkoa ni mjumbe wa kamati ya siasa mkoa hivyo, atawashangaa ambao watashangaa kumuona jukwaani akimnadi mgombea wa CCM.

Naye, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha, Loota Sanare alisema anawataka wananchi wa Monduli kumchagua Julius Kalanga na kuachana propaganda.

Alisema kama Lowassa angekuwa anawatakia maendeleo wananchi wa Monduli angegombea yeye ama mtoto wake, Fred Lowassa.

Aliwataka wakazi wa Monduli kutorejea makosa kuchagua upinzani kwani sasa wanapaswa kuonyesha wanamuunga mkono Rais John Magufuli kutokana na kazi nzuri anayofanya.

Meneja Kampeni za ubunge Monduli, William Ole Nasha alisema katika kampeni hizo wabunge 16 watashiriki kumnadi mgombea wakiwamo mawaziri.

Alisema Kalanga alikuwa na kila sababu kuhama Chadema kwani mambo mengi ya maendeleo ikiwemo kutatua kero za maji, umeme na migogoro ya ardhi yalikwama.

Akizindua kampeni, Mangula alisema kumekuwepo na maneno ambayo si sahihi  kuwa taratibu za chama zinakiukwa kupitishwa wagombea bila kura za maoni

"Hakuna taratibu zilizokiukwa, kama kunakuwa na mgombea mmoja hakuna haja ya kura za maoni," alisema.

Mangula alisema chama kinatazama mgombea ambaye anaungwa mkono na wengi na kueleza katika uchaguzi uliopita, Kalanga alipata kura 35,000 na kuwashinda wengine.

Mangula aliridhishwa na umati wa wanaccm waliojitokeza kwenye kampeni hizo na mapokezi makubwa waliyompa.

"Mwenyekiti wetu Rais John Magufuli aliniomba nije kuzindua kampeni na alinipa heshima kubwa na nyie nawashukuru kutuunga mkono," alisema.

Alisema katika uchaguzi huo hawashindanishi Ilani za uchaguzi kwani tayari ilani iliyopo ni ya CCM ambayo ndio mipango yake imepitishwa na wabunge.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara akisalimiana na Mgombea Ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi CCM Jimbo la Monduli, Bw.Julius Kalanga Laizer akisaimiana na wananchi waliofika katika mkutano wa uzinduzi wa Kampeni za ubunge jimbo la Monduli uliofanyika jana  jimboni humo.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara akimnadi  Mgombea Ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi CCM  Jimbo la Monduli, Bw.Julius Kalanga Laizer akisaimiana na wananchi waliofika katika mkutano wa uzinduzi wa Kampeni za ubunge jimbo la Monduli uliofanyika jana jimboni humo.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara akihutubia wananchi katika mkutano wa kampeni  za Ubunge Jimbo la Monduli, Bw. Julius Kalanga Laizer akisaimiana na wananchi waliofika katika mkutano wa uzinduzi wa Kampeni za ubunge jimbo la Monduli uliofanyika jana  jimboni humo.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za ubunge jimbo la Monduli jana

No comments

Karibu tena,asante kwa kusoma habari hii!