Header Ads

SHIRIKA LA KIMATAIFA LA WATER MISSION TANZANIA LAFANIKISHA MRADI WA MAJI SAFI NA SALAMA KIJIJI CHA KASANDA- KIGOMA

Kiongozi wa mbio za mwenge,Charles Kabeho akifungua bomba kuashiria uzinduzi wa mradi wa maji wa Kasanda iliofadhiliwa na Water Mission Tanzania.
Shamrashamra za uzinduzi wa mradi
Kiongozi wa mbio za mwenge, Charles Kabeho, akiongea na wananchi wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji Kasanda,(kushoto) ni Mkurugenzi wa Kanda wa shirika la kimataifa la Water Mission, Will Furlong
Wakazi wa kata ya Kasanda, wilayani Kakonko mkoani Kigoma, jana,wameanza kupata maji safi na salama kutokana na kuzinduliwa kwa mradi mpya wa maji chini ya ufadhili wa Shirika la kimataifa la Water Mission Tanzania. Mradi huu utanufaisha zaidi ya kaya 729 zinazoishi maeneo hayo.
Miradi ya Kakonko na Kasanda, ni miongoni mwa miradi zaidi ya 20 ya kuwapatia wananchi maji safi na salama ambayo imetekelezwa na shirika la Water Mission Tanzania tangu mwaka 2014. Miradi ya Kasanda na Kakonko ni tofauti na ile iliyotekelezwa maeneo mengine kwa kuwa iko katika maeneo yaliyopo karibu na kambi ya wakimbizi ya Mtendeli.
Mkurugenzi wa Kanda wa shirika la kimataifa la Water Mission, Will Furlong alisema “Water Mission Tanzania, kupitia ufadhili wa taasisi ya Poul Due Jensen Foundation ambayo zaidi inajulikana kama, Grundfos Foundation, imewezesha ufanikishaji miradi 8 ya maji safi na salama kwa jamii mbalimbali nchini. Mradi mwingine wa Zeze mkoani Kigoma nao tayari umezinduliwa mwezi huu. Mashirika ya Water Mission Tanzania na Grundfos Foundation, yanashirikiana kuhakikisha huduma za maji safi na salama zinafikia jamii zenye changamoto katika kanda ya Afrika Mashariki”.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa mradi huu mkubwa wa maji ulioambatana na sherehe za mbio za Mwenge katika kata hiyo,Kiongozi wa mbio za mwenge,Charles Kabeho,alisema kuwa kuzinduliwa kwa mradi huo ni jambo la kihistoria kwa wakazi wa eneo hilo ambalo kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kupata maji safi na salama.
“Kwa niaba ya serikali napenda kutoa shukrani kwa wadau wa maendeleo wanaounga mkono jitihada za serikali katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokabili jamii kama ambavyo hawa wenzetu wa Water Mission Tanzania ,wamekuwa mstari wa mbele kufanikisha miradi ya maji sehemu mbalimbali hapa nchini”alisema Kabeho.
Alisema kero ya ukosefu wa maji safi na salama kwa muda mrefu ilisababisha akina mama kutembea mwendo mrefu kutafuta maji sambamba na wananchi wengi kuathirika kwa kupata magonjwa mbalimbali kutokana na kutumia maji yasio salama kwa matumizi ya binadamu.
Kabeho,alitoa wito kwa wakazi wote wa eneo hilo kujiona ni sehemu ya mradi huu na kuhakikisha wanatunza miundo mbinu ya mradi wakati wote sambamba na kutoa ushirikiano kwa wataalamu wanaofanya ushauri wa uendeshaji mradi.

No comments

Karibu tena,asante kwa kusoma habari hii!