Header Ads

WAZIRI WA JK AREJEA CCM ATWAE JIMBO 2020

Mwanasiasa wa upinzani na aliyekuwa Naibu Waziri katika serikali ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Goodluck Ole Medeye, ametangaza kurejea Chama Cha Mapinduzi huku akidai kuwa ameamua kufanya hivyo kwa kuwa vitendo vya rushwa,-Hususan nyakati za uchaguzi, vimemalizwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Dk. John Magufuli.
Ole Medeye juzi alisema kilichomkimbiza CCM mwaka 2015 na kujiunga na Chadema ni vitendo vya rushwa katika mchakato wa kupata wagombea wa chama hicho tawala.
Alisema anafurahi kuona sasa vitendo hivyo havipo ndani ya CCM baada ya kudhibitiwa na Rais Magufuli.Ole Medeye alikuwa mmoja wa wabunge watano wa CCM waliojiunga na Chadema Agosti 12, 2015 wakiongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (Monduli). 
Ole Medeye aliteuliwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuwania nafasi ya Uspika wa Bunge baada ya Uchaguzi Mkuu.
Wengine waliohama pamoja na Lowassa ni Makongoro Mahanga (Segerea), James Lembeli (Kahama) na mbunge wa viti maalum, Esther Bulaya ambaye sasa ni mwakilishi wa wananchi wa Bunda Mjini (Chadema).
Hata hivyo, Ole Medeye alihama Chadema kabla ya mwaka kumalizika na kujiunga na UDP kinachoongozwa na John Cheyo Juni 12, 2016.
Medeye alisema alihamia UDP kwa kuwa inasimamia haki na demokrasia na kwamba yeye alikuwa akitaka demokrasia ya kweli na jukwaa la haki katika kuleta haki na maendeleo kwa Watanzania.
Alisema kuwa alikaa chama hicho cha 'Bwana Mapesa' kwa miezi mitatu tu hata hivyo, kwa kuwa "nilikwenda kufanya kazi maalum."
Na sasa, Ole Medeye amesema ameamua kurejea CCM kwa kuwa kila mwanachama anayo fursa kushiriki uchaguzi, ikiwamo kugombea nafasi yoyote bila kutoa rushwa na akashinda.
"Mimi sijawahi kuwahonga watu ili wanichague," alisema Ole Mideye na "wakati huo CCM kulikuwa na rushwa sana; ndiyo maana nikaamua kukimbia.
"Lakini kwa sasa hakuna tena kitu kama hicho, hivyo nimeamua kurejea CCM."
Ole Medeye alisema katika Uchaguzi Mkuu ujao, mwaka 2020, anataka kurudi na kuwatumikia wananchi kupitia nafasi ya ubunge.

No comments

Karibu tena,asante kwa kusoma habari hii!