Header Ads

WABUNGE KUSIMAMIA UUNDWAJI WA KANUNI NA SHERIA ZA KUTUNZA VYURA WA KIHANSI


WABUNGE wameahidi kusimamia uundwaji wa kanuni na sheria za kutunza vyura wa Kihansi ambao ni wa kipekee duniani baada ya kukamilika kwa mradi wa kuwatunza.

Wakiwa katika ziara iliyoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais wiki iliyopita, wabunge hao kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara na Mazingira, walisema vyura hao wanagusa maisha ya watu wengi hasa ikizingatiwa wakazi wa eneo hilo wanayahitaji mazingira na viumbe vyake.

Kaimu mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Igunga, Dk. Dalali Kafumu, alisema juhudi lazima zifanyike kuhakikisha vyura hao wanabaki salama, lakini wakati huohuo shughuli za kijamii ziendelee ikiwamo kuzalisha umeme.

“Tumekuja kujifunza masuala ya mazingira ambayo yanahusiana na viwanda, mradi tuliokuja kutembelea unahusisha wadau wengi kwa sababu vyura hawa adimu lazima watunzwe na umeme lazima uzalishwe,” alisema Dk. Kafumu.

Alibainisha kuwa wanajipanga kutunga sheria na kanuni za kuwalinda viumbe waliozunguka eneo la Kihansi na wameelezwa kuna viumbe hai vingi vya kipekee visivyopatikana ulimwenguni kote zaidi ya hapo.

“Wanavijiji na wadau wengine wakiwamo watafiti wa vyuo vikuu kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) wana nafasi kubwa ya kuhifadhi eneo hili muhimu kwa nchi yetu,” alisema na kuongeza:

"Wabunge tutatimiza wajibu kwa kusimamia uundwaji wa kanuni za kuwalinda na ndiyo maana tumekuja kujifunza ukubwa wa mradi huu ili tukiwa bungeni tujue namna ya kuutetea. Ni muhimu serikali iuchukue huu mradi maana tumeambiwa unaisha mwakani."

Awali akiwakaribisha wabunge hao, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Vedast Makota, alisema kwa sasa shughuli ya uhifadhi wa viumbe hao zinafanywa kwa kushirikisha wananchi na watafiti wa vyuo vikuu pamoja na Shirika la Umeme (Tanesco).

“Tuna vifaa vingi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya kuwapokea vyura wanaotoka nje walikokwenda kuhifadhiwa, vilevile wakija Kihansi kuna vifaa vingine tunawapokea katika kituo hiki kikubwa ambacho awali kilikuwa chini ya NEMC, lakini hawa ni wanyama, wapo chini ya maliasili na wilaya zilizozunguka eneo hili za Mufindi, Kilolo na Kilombero,” alisema Dk. Makota.

Katika ziara hiyo, Mbunge wa Singida Mjini, Mussa Sima, alisema Watanzania hawana budi kujivunia viumbe hao adimu kwa kushikamana kuwaokoa.

“Tumeona wizara imeamua kufanya kazi hii kwa vitendo, Watanzania tunapaswa kujivunia uwapo wa vyura hawa. Kamati ya Bunge tutashiriki kwa kutengeneza kanuni ili kuwalinda. Kimsingi ipo faida ya kiuchumi kama utalii na kutunza mazingira na viumbe hai, ni faida kubwa. Natoa rai wananchi wanaozunguka eneo hili mbali ya kupata elimu lakini washiriki kuwatunza viumbe hawa ambao ni adimu,” alisema Sima.

No comments

Karibu tena,asante kwa kusoma habari hii!