Header Ads

SHERIA KALI YAANDALIWA KULINDA MISITU NCHINI

SERIKALI kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi wa misitu na bayoanui, inakamilisha taratibu za kutungwa sheria mpya pamoja na kanuni zake ili kudhibiti uharibifu wa misitu nchini.

Hatua hiyo inakuja kutokana na sheria zilizokuwepo kupitwa na wakati na kuchangia kuharibika kwa misitu kila mwaka.

Maamuzi ya kuanzisha sheria hiyo mpya yamekuja kutoka na sekta ya misitu na nyuki hapa nchini kuwa katika hatari ya kutoweka hali inayochangiwa kwa asilimia kubwa na vitendo vya uchomaji wa mkaa pamoja na ukataji kuni.

Akizindua mchakato wa kuhakiki rasimu ya taifa ya misitu, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga, alisema maamuzi ya kutunga sheria mpya yanatokana na ile iliyopo ya mwaka 1998 kutokuendana na mabadiliko ya jamii ya sasa ambayo yanatishia kwa kasi uhai wa sekta hiyo ya misitu.

Naibu Waziri alisema sekta ya misitu na nyuki ni mtambuka kwani inashirikisha wizara mbalimbali kama Nishati, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),Afya, Viwanda na Biashara hivyo kulingana na sheria mpya kazi ya kulinda misitu itakuwa ikifanywa kwa pamoja.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS),Profesa Dos Santos Silayo, alisema kuanzishwa kwa sheria hiyo mpya itakuwa mkombozi wa misitu nchini kwa kuwa iliyopo ilitoa mwanya kwa baadhi ya watu kufanya uharibifu.

Alisema kuwa rasilimali za misitu zipo za kutosha kulingana na ikolojia mbalimbali za kila eneo kama kuweka sheria kali za kuhifadhi kuna hatari ya vizazi vijavyo vikashindwa kuzitumia rasilimali hizo.

Mtalaam wa misitu, Dk. Felician Kilahama,alisema kuwa sekta ya misitu inakabiliwa na changamoto kubwa ya usimamizi,ukataji wa miti ambapo katika kipindi cha miaka mitatu iliopita hekta 582 zilifanyiwa uharibifu kwa ajili ya shughuli za uchomaji wa mikaa na ukataji wa kuni.

Alisema kuwa kuanzishwa kwa sheria hiyo mpya ya misitu na kusimamiwa kwa pamoja , serikali pamoja na wadau kutawezesha kurudisha misitu ya asili kwa haraka ambayo imeanza kutoweka kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira.

No comments

Karibu tena,asante kwa kusoma habari hii!