Header Ads

SAUDI ARABIA: WANAWAKE WAINGIA UWANJANI KWA MARA YA KWANZA

Jana ilikuwa ni siku ya kihistoria ya soka la nchi ya Saudi Arabia baada ya wanawake nchini humo kuhudhuria mechi ya soka kwa mara ya kwanza.

Ilikuwa majira ya saa 2:00 usiku kwenye uwanja wa Mfalme Abdullah jijini Jedda, wanawake walikuwa tayari uwanjani wakitazama mechi ya ligi kuu kati ya Al-Ahli dhidi ya Al-Batin ambapo Al Ahli ilishinda mabao 5-0 na kuendelea kusalia katika nafasi ya 2 kwenye msimamo wa ligi hiyo yenye timu 14 huku Al-Batin ikibaki katika nafasi ya tisa.

Ruhusa ya wanawake kuingia uwanjani ilitolewa mwezi Oktoba mwaka jana na Mtawala wa sasa wa nchi hiyo (Crown Prince Mohammad Bin Salman Al Saud) ikiwa ni sehemu ya mabadiliko makubwa yanayofanyika nchini humo yanayolenga kuleta haki na usawa kati ya mwanamke na mwanaume katika baadhi ya maeneo.

Hata hivyo wanawake wametengewa jukwaa lao "Family sections" ambapo wataruhusiwa kukaa na familia zao bila kuchanganyikana na wanaume ambao si wa familia zao. Baada ya mechi ya jana usiku pia kesho kutakuwa na mechi kwenye uwanja wa Mfalme Fahd jijini Riyadh ambapo pia wametengewa jukwaa maalum.

Alhamisi ijayo pia wanawake watapata nafasi ya kuhudhuria mechi kwenye uwanja wa Prince Mohammed bin Fahd mjini Dammam wakiketi na familia zao kama ilivyokuwa jana. Mwaka jana pia serikali ilitoa ruhusa ya wanawake kuanza kuendesha gari katika shughuli zao mbalimbali za kila siku.

No comments

Karibu tena,asante kwa kusoma habari hii!