Header Ads

KAPTENI WA JWTZ ADAIWA KUMUUA ASKARI POLISI KWA KUMPIGA NGUMI NA MATEKE BAA

OFISA wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kapteni Sudy Hussein (32) anashikiliwa na Polisi Kibaha, mkoani Pwani kwa tuhuma za kusababisha kifo cha Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Polisi (ASP), Lawrence Minja (58) akidaiwa kumpiga ngumi na mateke.

Habari zilizopatikana Dar es Salaam jana na kuthibitishwa na Polisi, zilidai tukio hilo lilitokea wakati wa mkesha wa Krismasi. Lilitokea wakati maofisa hao walipokuwa wakipata vinywaji katika ‘baa’ moja Picha ya Ndege, kabla ya kujitokeza malumbano kati ya mhudumu wa baa hiyo na mmoja wa wanawake, aliyekuwa ameambatana na ofisa huyo wa JWTZ, Kambi ya Jenerali Twalipo, Mgulani, Dar es Salaam.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, ASP Blasius Chatanda alithibitisha tukio hilo, akisema mwili wa marehemu uliagwa jana. 

Kamanda Chatanda alisema Minja alipigwa baada ya mzozo wa malipo ya bia uliohusisha mwanamke aliyekuwa na Kapteni na mhudumu wa baa baada ya kutaka kulipa kwa Tigo- Pesa.

Kamanda alisema baada ya mhudumu kudai hapokei malipo kwa Tigo-Pesa, kulitokea ubishi uliomfanya ASP Minja kusogea kuwasuluhisha. “Huyu mwanamke aliyekuwa ameongozana na ofisa wa jeshi alikuwa akilazimisha kulipa ‘bili’ yake kwa simu huku mhudumu akikataa akitaka ‘cash’ (fedha taslimu).

Baada ya ofisa wetu (Minja) kuona hivyo, aliingilia kati kusuluhisha hali ikawa shwari,” alisema Kamanda Chatanda. Alisema wakati Minja akiamini hali ni shwari, Kapteni Sudy anadaiwa kusimama ghafla kutoka meza aliyokuwa amekaa na kumfuata Minja na kumshambulia kwa ngumi na mateke sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababisha aanguke chini na kupoteza fahamu.

Alisema baada ya watu waliokuwa karibu kuona hali hiyo, walimchukua Minja kumpeleka Hospitali ya Tumbi kwa matibabu, wengine wakishirikiana kumkamata Kapteni huyo na kumpeleka Polisi alikofunguliwa mashitaka.

Kamanda Chatanda alisema baada ya Minja kufikishwa Tumbi, alikaa hapo kwa siku mbili hadi Desemba 26, 2017 aliporuhusiwa kurudi nyumbani huku mshitakiwa akipewa dhamana, huku wakifuatilia afya ya Minja, ambayo wakati huo ilionekana ya kuridhisha kiasi fulani.

“Lakini ilipofika Desemba 27 hali ya Minja ilibadilika tena, wakati huu ikionekana mbaya zaidi, hatua iliyofanya akimbizwe Hospitali ya Mloganzila na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Kitengo cha Mifupa, MOI, kwa matibabu zaidi akionekena amepoteza kumbukumbu,” alisema Kamanda Chatanda.

Alisema kipindi chote Minja alipokuwa hospitalini hapo, alilazwa kitengo cha watu wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) huku hali yake ikizidi kuwa mbaya kadiri siku zilivyozidi kusogea hadi alipofariki Ijumaa Januari 12, mwaka huu.

Kamanda Chatanda alisema baada ya kifo hicho, waliwasiliana na JWTZ na kutoa taarifa hiyo ili waweze kukabidhiwa ofisa huyo wa jeshi, kwa hatua za kisheria kwa kusababisha kifo cha ofisa wa Polisi na kuzuia asitoroke.

“Wenzetu JWTZ walitutaarifu, tayari hilo limetekelezeka na sasa anashikiliwa huko huko jeshini wakati tukifanya utaratibu wa kumleta huku kwa hatua zaidi. Tunasubiri tumalize msiba huu ili tuendelee naye,” alisema. Alisema marehemu ASP Minja alisafirishwa jana kwenda kijiji cha Komela, Marangu mkoani Kilimanjaro kwa maziko leo.

IMEANDIKWA NA OSCAR JOB - habarileo

No comments

Karibu tena,asante kwa kusoma habari hii!