Header Ads

HATIMA YA WALIOFUKUZWA KWA VYETI FEKI, WENYE VYETI VYA DARASA LA 7 NA KUHHUSU KUPANDISHWA MADARAJA

HATIMA ya mafao ya wafanyakazi wa serikali walioondolewa kwenye ajira kutokana na kubainika kuwa na vyeti feki itajulikana kabla ya Bunge la Bajeti, imefahamika.

Hatua hiyo inatokana na serikali kujibu hoja nane za Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) na kwamba suala la kulipwa au kutolipwa haki zao litafahamika Machi au Aprili, mwaka huu.

Hoja zingine ni ajira ya waliomaliza darasa la saba, kupandishwa madaraja, madeni ya wafanyakazi, nyongeza za mishahara, kutofanyika vikao vya bodi, kujua idadi ya taasisi zilizoundwa na kuunganishwa kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Katibu Mkuu wa Tucta, Dk. Yahya Msigwa, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa mamlaka mbalimbali zinamalizia kulifanyia kazi suala la vyeti feki na kwamba kabla ya Mei Mosi, mwaka huu, hatima yao itakuwa imepatikana.

“Unajua kilichofanyika ni kosa la jinai na la kinidhamu, hivyo sisi Tucta tunaendelea kuiomba serikali angalau wapatiwe kifuta machozi,” alisema.

Alisema ajira kwa waliomaliza darasa la saba Serikali ilitoa waraka unaosema watumishi wa umma wanapaswa kumaliza elimu ya kidato cha nne kuanzia Mei, 20, 2004.

Pia alisema baada ya hapo, walitakiwa kujiendeleza ili kuwa na vigezo vya kuendelea kuwa watumishi wa umma iwapo zipo baadhi ya idara zinawahitaji na kujenga hoja.

Kuhusu kupandishwa madaraja,
Dk. Msigwa alisema watumishi wengi hawajapandishwa kutokana na uhakiki wa vyeti, hivyo serikali imetenga fedha kwa ajili ya mpango huo kwa kutegemea bajeti ijayo.

Alisema malipo yataanza tangu siku ya kupata barua ili kupunguza madeni ambayo inadaiwa na kwamba kimsingi katika hilo, yako madeni ya mishahara na isiyo ya mishahara.

Kuhusu madeni, kwa mujibu wa Dk. Msigwa, serikali imesema imemaliza uhakiki na imeanza kulipa lakini itakuwa vigumu kulipa watu wote kwa mkupuo bali watazingatia uhakiki ya madeni yenyewe.

Kwa upande wa nyongeza ya mishahara, alisema Rais John Magufuli hakuahidi wakati wa sherehe za Mei Mosi bali nyongeza hiyo italolewa mwaka huu.

Aidha, Dk. Msigwa alisema hoja ya kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa na mifuko miwili, mmoja wa binafsi na mwingine wa umma, imetokana kauli za wafanyakazi wenyewe kwenye sherere za Mei Mosi.

Alisema rasimu iliyotegenezwa si mbaya licha upungufu uliopo na wanaendelea kutoa maoni kabla muswada haujawasilishwa Bungeni.

No comments

Karibu tena,asante kwa kusoma habari hii!