Header Ads

AIRTEL YAIJIBU SERIKALI, YADAI TARATIBU ZOTE ZILIFUATWA WAKATI WA UBINAFISISHAJI

Kampuni ya Bharti Airtel inayomiliki kampuni ya Airtel Tanzania, imeeleza kusikitishwa kwake na taarifa ya kamati iliyoundwa kuchunguza umiliki wake iliyotolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango juzi.

Taarifa ya Bharti iliyotolewa jana imeeleza kuwa uwekezaji wake ulifuata na kuzingatia sheria na taratibu zote za nchi kabla ya baraka za Serikali ya Tanzania.

Juzi, Waziri Mpango aliwasilisha kwa Rais John Magufuli taarifa ya kamati iliyoundwa kuchunguza umiliki wa kampuni ya simu ya Airtel na kueleza jinsi sheria na taratibu zilivyokiukwa katika ubinafsishaji wake.

Kutokana na ukiukwaji huo, Dk Mpango alisema Serikali inayomiliki asilimia 40 ya hisa za kampuni ya Airtel imeamua kufanya mazungumzo na kampuni ya Airtel inayomiliki asilimia 60 ya hisa ili nchi iweze kupata haki yake.

“Lakini niwaambie Watanzania yale ambayo tumeyaona ni machafu sana, ni mambo ya hovyo kabisa, nchi yetu kwa kifupi tuliingizwa mkenge, ni fedha nyingi zimepotea kwa hiyo sisi katika majadiliano haya lengo letu litakuwa ni kuhakikisha Watanzania wanapata haki yao” alisema. 
Waziri Mpango aliunda kamati hiyo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli la Desemba 20 mwaka jana wakati akiweka jiwe la msingi katika jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mjini Dodoma.

Lakini katika taarifa yake ya jana, Bharti imeonyesha mlolongo wa miamala na matukio kadhaa wakati wa ubinafsishaji ikidai kuwa hiyo inaweza ikaonyesha uwazi uliokuwapo.

Mchakato huo ni ule wa kuanzia kutafutwa kwa mwekezaji ndani ya TTCL kwa ajili huduma za simu za mkononi mwaka 2001 hadi uuzwaji wa Zain kwenda Airtel.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa katika kila hatua, Serikali ilikuwa ikishirikishwa na kulikuwa na uwazi mkubwa na matakwa yote ya kisheria yalikuwa yakifuatwa.

“Miamala yote ilikuwa ikifanyika chini ya usimamizi wa bodi ya wanahisa wa MSI, wawakilishi wa Benki ya Dunia, Serikali ya Uingereza, Marekani, Uholanzi na Ujerumani. Makundi hayo ya watu yalishirikishwa ili kuhakikisha maadili na misingi ya utawala bora katika kampuni,” inaeleza taarifa hiyo.

Imemuomba Waziri Mpango kuipatia matokeo ya kamati hiyo kuhusiana na ubinafsishaji wake ili kama kuna hoja zozote iweze kuzijibu kwa hoja kutokana na kumbukumbu za kampuni.

No comments

Karibu tena,asante kwa kusoma habari hii!